Friday, November 1, 2013

SOMA HAPA: MBINU ILIYOTUMIKA KUIBA TWIGA TANZANIA



Moshi na Dodoma. Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi, imeelezwa kuwa marubani wa ndege ya kijeshi ya Qatar, walitumika katika kutorosha twiga wanne kwenda Uarabuni na kwamba washtakiwa walikuwa na hati za kusafiria zenye hadhi ya kidiplomasia.

Shahidi wa 13, Prisca Sabugo ambaye ni Ofisa Uhamiaji, aliiambia mahakama juzi kuwa hati hizo hazikugongwa mihuri wala kupewa viza.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Kobelo, shahidi huyo alidai kuwa ndege hiyo ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) Novemba 24 mwaka 2011.

“Baada ya hiyo ndege ya jeshi kutua, alikuja wakala wao kutoka Kampuni ya Equity Aviation akaniletea Diplomatic Passport zao na akaniambia wamekuja kwa shughuli za utalii kwa siku tatu,” alisema.

Huku akiongozwa na mawakili wa Serikali, Evetha Mushi na Joseph Maugo, shahidi huyo alidai kuwa marubani na wafanyakazi wa ndege huwa hawapitii utaratibu wa kawaida wa kujaza fomu na kupewa viza. Alisema, tangu wageni hao waingie nchini kama watalii, hawakuwahi kuhojiwa na chombo chochote kuhusu kutogongwa mihuri kwenye hati zao.

Shahidi wa 12, Oscar Jullius ambaye ni Ofisa Wanyamapori, alidai kuwa vibali vilivyotumika kukamata wanyama hao vilikuwa vya kampuni mbili ambazo ni Ham Market na Luega Birds Traders.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, vibali hivyo vilikuwa vya kumiliki nyara na si vya kukamata wanyamapori hai na kwamba yeye ndiye aliyeandika ripoti ya thamani ya wanyama hao.

Alisema thamani ya wanyama wote waliotoroshwa ilikuwa ni Sh170.5 milioni na kwamba twiga hao wanne kila mmoja alikuwa na thamani ya Dola 10,000 za Marekani sawa Sh60 milioni za Tanzania.

Alipoulizwa na mmoja wa mawakili wanaowatetea washtakiwa, Edmund Ngemela, kama vibali walivyokuwa navyo vilikuwa halali, alikiri kuwa vilikuwa halali na vilikuwa ni vya kumiliki nyara.

Kesi hiyo imepangwa kuendelea Novemba 29 mwaka huu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na raia wa Pakistan, Kamran Ahmed, Hawa Mang’unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu ambao wote wako nje kwa dhamana.

Katika hatua nyingine, madiwani watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro akiwamo mwenyekiti wa halmashauri hiyo, wanashikiliwa na maofisa wa Kikosi cha Maalumu cha Kupambana na ujangili.

No comments:

Post a Comment

PLEASE LEAVE YOUR COMMENTS HERE. HELP BLOG DEVELOPMENT

Print It: