Thursday, January 2, 2014

HOTUBA YA RAISI KIKWETE, UJENZI WA MIUNDO MBINU NA NISHATI

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,

TAREHE 31 DESEMBA, 2013

CONTINUED



Ujenzi wa Miundombinu
Ndugu wananchi;
          Katika mwaka 2013, tumeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani. Kasi ya ujenzi wa barabara imeendelea kufanyika kote nchini. Kazi ya ujenzi ingekuwa nzuri zaidi kama mtiririko wa malipo kwa Wakandarasi ungekuwa mzuri.  Tatizo hili tutalitafutia ufumbuzi mwaka 2014 ili kasi ya ujenzi wa barabara za lami nchini iwe nzuri zaidi.
Pamoja na hayo mwaka huu kilomita 877 za barabara zimekamilika. Ujenzi wa daraja la Malagarasi nao umekamilika kinachosubiriwa ni sherehe za uzinduzi. Ujenzi wa daraja la Kilombero umeanza na ule wa daraja la Kigamboni unaendelea vizuri. Tunatarajia kuwa mwakani tutaongeza zaidi kasi ya ujenzi wa barabara zilizosalia ikiwa ni pamoja na kujenga baadhi ya barabara kwa ubia na sekta binafsi.  Kwa kasi na mwenendo tunaoendelea nao sasa naamini ifikapo mwaka 2015 tutakuwa tumefikia hatua ya juu sana katika shabaha yetu ya kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami.   
Ndugu Wananchi;
          Jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam zimeendelea kutekelezwa.  Barabara kadhaa zilipanuliwa na kazi inaendelea.  Ujenzi wa njia ya kupita mabasi yaendayo haraka umeendelea kwa kasi ya kuridhisha.  Mchakato wa ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika njia panda za TAZARA na Ubungo umeshaanza.  Mwaka ujao huduma ya usafiri wa treni kusafirisha abiria Dar es Salaam itaongezwa ili watu wengi zaidi wanufaike.
Ndugu wananchi;
          Mwaka huu, kwa upande wa reli ya kati, kazi ya kuboresha njia ya reli imeendelea kufanyika na itaendelea mwaka 2014.  Mwakani (2014) Shirika la Reli litapokea injini mpya 13, mabehewa ya mizigo 274 na breki 34 hivyo kuboresha sana huduma katika reli ya kati.  Kuhusu ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa ni matarajio yetu kuwa kama kila kitu kitaenda sawa mchakato wa ujenzi utaanza katika nusu ya pili ya mwaka 2014.
Ndugu Wananchi;
Tumetoa kipaumbele cha juu katika kuboresha huduma ya usafiri wa anga nchini.  Mwaka huu, tumeendelea na ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mikoa ya Kilimanjaro, Kigoma, Tabora, Mwanza, Arusha, Mtwara na Kagera.  Ni jambo la kufurahisha kuona Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe ukianza kutumika. Hatimaye ndoto imetimia.  Mwaka wa 2014 ujenzi wa majengo mengine ya kuhudumia abiria, mizigo na ndege utaendelea katika uwanja huo.
Pia ni furaha iliyoje kwamba upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na ujenzi wa gati la Kilindoni vimekamilika.  Kero ya miaka mingi imepatiwa ufumbuzi.  Kazi ya ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere itaanza rasmi mwaka 2014. 
Nishati
Ndugu wananchi;
          Dhamira yetu ya kutaka Tanzania iwe na umeme wa uhakika na unaonufaisha watu wengi imepata sura na mwelekeo mzuri mwaka huu 2013.  Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam umeanza na utekelezaji unakwenda vizuri.  Kama ujenzi wa bomba utakamilika kama inavyotarajiwa na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi utaenda kama ilivyopangwa, ifikapo mwaka 2015 Tanzania itafikia lengo la kuzalisha megawati 3,000 za umeme.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri mwaka huu, kufuatia kuongezewa fedha za bajeti, kasi ya usambazaji umeme imekuwa nzuri.  Tunaumaliza mwaka huku idadi ya Watanzania waliounganishiwa umeme ikiwa imefikia asilimia 24 ukilinganisha na asilimia 21 mwaka 2012 na asilimia 10 mwaka 2005. Haya si mafanikio madogo. Kwa mwelekeo huu, kufikia lengo la asilimia 30 ya Watanzania kupata umeme mwaka 2015 ni jambo la uhakika kabisa sasa. Tena kuna uwezekano mkubwa wa kulivuka lengo hilo.  
Endelea USHIRIKIANO WA KANDA NA EAC 

No comments:

Post a Comment

PLEASE LEAVE YOUR COMMENTS HERE. HELP BLOG DEVELOPMENT

Print It: