Tuesday, October 29, 2013

PENSHENI ZA WASTAAFU SERIKALINI NI AIBU


Kama kuna watumishi wa umma ambao mara wanapostaafu wanaishi maisha ya udhalilishaji kutokana na kulipwa pensheni isiyoendana na hali ngumu ya maisha, watumishi hao ni wale waliokuwa katika ajira mbalimbali serikalini katika ngazi za chini na kati. Tofauti na pensheni za wastaafu wa ngazi za juu, wengi wao hupata pensheni ya Sh50,000 kila mwezi ambazo hata kwa kujibana kupita kiasi haitoshelezi mahitaji ya siku tano.

Ndiyo maana wananchi wengi wiki iliyopita walipinga kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda aliposema wabunge wanapomaliza vipindi vyao bungeni wanakuwa ombaomba kutokana na mishahara yao kuwa midogo. Spika huyo alisema ofisi yake inaandaa utaratibu wa kuanzisha mafunzo ya ujasiriamali kwa wabunge wote ili wawe na kazi ya kuwaingizia kipato mara baada ya kustaafu.

Hoja kuu ya wanaopinga kauli ya Spika Makinda ni kwamba mishahara ya wabunge ni mikubwa sana hata bila kuweka posho na marupurupu mengine mengi wanayopata. Kwa wastani tu, mshahara wa mbunge kwa mwaka ni zaidi ya Sh660 milioni. Makadirio ya kiinua mgongo, posho na marupurupu hayapungui Sh280 milioni. Mapato hayo ni nje ya fedha anazokopeshwa na Bunge ambazo zinamwezesha kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kibiashara.

Tunasema fedha hizo ni nyingi mno katika kipindi kimoja cha miaka mitano, hivyo mbunge anayemaliza muda wake na kuishi maisha ya ombaomba anakuwa ametumia fedha hizo vibaya tofauti na mtumishi wa Serikali wa ngazi hizo tulizozitaja ambazo mshahara wake mdogo ndiyo unaosababisha alipwe pensheni ya udhalilishaji ya Sh50,000 kila mwezi. Ni hali inayoeleweka mtumishi huyo anapoishi maisha ya ombaomba na kuhangaika, kwani kipato chake katika muda wote anapokuwa katika ajira ya Serikali hakimpi uhakika wa maisha bora baada ya kustaafu.

Siyo siri kwamba zaidi ya asilimia 80 ya watumishi wa Serikali hulipwa mishahara midogo, hivyo na pensheni zao huwa kiduchu mara wanapostaafu. Wengi hulazimika kutumia gharama kubwa kusafiri umbali mrefu kufuata pensheni zao katika vituo vilivyopangwa na wakati mwingine huzipata baada ya kukaa siku mbili hata tatu. Wakati huohuo, kuna sera kwamba wastaafu serikalini wapewe matibabu bure, lakini hili linashindikana kutokana na uhaba mkubwa wa dawa katika hospitali na vituo vya afya vya Serikali. Kukosekana kwa huduma za afya kunadhoofisha afya za wastaafu wengi na matokeo yake ni kuandamwa na magonjwa na hatimaye kupoteza maisha.

Wengi ni watumishi ambao hawana vitendea kazi vya kutosha wala marupurupu zaidi ya kubebeshwa lawama na malalamiko yasiyoisha. Matokeo yake ni kukata tamaa na kujiona watu dhaifu, huku wakifanya kazi kwa kusuasua wakisubiri kustaafu katika mazingira ya huzuni na unyonge. Hawa ndiyo watumishi wanaostahili kuwezeshwa na Serikali ili wajiongezee kipato kwa kupewa mikopo ya masharti nafuu.

Licha ya umuhimu wa Serikali kuboresha pensheni zao kwa viwango stahiki, hawa ndiyo watumishi wanaostahili kugharimiwa na fedha za umma kwa kupewa mafunzo na mitaji ya kuwawezesha kufanya ujasiriamali ili kuepuka kuishi maisha ya aibu. Inawezekana kabisa kuwainua watumishi hawa kiuchumi kabla na baada ya kustaafu. Ipo miradi mingi wanayoweza kusaidiwa kuianzisha na kuiendesha, ikiwa ni pamoja na ufugaji na kilimo cha mboga za majani.

SOURCE: Mwananchi Communication LTD

No comments:

Post a Comment

PLEASE LEAVE YOUR COMMENTS HERE. HELP BLOG DEVELOPMENT

Print It: