Tuesday, October 29, 2013

Polisi Tanga waua wawili mapambano na raia


Kilindi. Watu wawili akiwamo Imamu wa Msikiti wa Kitongoji cha Madina, mkoani Tanga, wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi kwa kile kilichoelezwa ni mapambano kati ya polisi na watu hao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema jana kwenye eneo la tukio kuwa, polisi waliwakabili watu hao kwa bunduki baada ya kuonyesha nia ya kutaka kuwadhuru askari walipokuwa kazini.

Massawe alisema tukio hilo limetokea wakati polisi walipokwenda Kijiji cha Kimamba kuwakamata washukiwa wa mauaji ya mgambo Salum Mgonje, wiki iliyopita.

Mgambo huyo aliuawa na wananchi ambao wengi ni wafanyabiashara waliokuwa wakipinga kutozwa ushuru wa mazao. Kutokana na mauaji hayo askari hao walifanya operesheni maalumu kusaka washukiwa wa mauaji yaliyotekelezwa Kijiji cha Lulago, Kata ya Lwande, wilayani hapa.

Katika vurugu hizo, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Songe, Edward Lusekelo alijeruhiwa kwa risasi. Mpaka sasa, wanavijiji 44 wa kata za Lwande na Negero wakiwamo wanawake na watoto wanashikiliwa na polisi. Akitoa maelezo ya mkasa huo wa Ijumaa iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa alisema hali kwenye vijiji hivyo imetulia.

Galawa aliwataja wanavijiji waliouawa katika mapambano hayo kuwa, ni Hamis Ramadhan mkazi wa Kijiji cha Negero na mfanyabiashara wa madini na ambaye hajatambuliwa ingawa ilielezwa kuwa alikuwa Imamu wa Msikiti na Mwalimu wa Madrasa katika msikiti uliopo Kitongoji cha Madina, Kijiji cha Kimamba, Kata ya Negero.

Gallawa alisema katika operesheni hiyo askari na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga, walikwenda vijiji mbalimbali na kukuta watu wengi wamekimbilia msituni kujificha vurugu.

“Katika operesheni hii, tulikwenda msituni na tukabaini vitongoji ambavyo walikuwa wakiishi Waislamu hawa wenye siasa kali, ambao kutokana na taarifa za kijijini walikuwa washukiwa wa vurugu zilizotokea na kusababisha mauaji ya mgambo na kujeruhiwa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Songe,” alisema.

Alitaja vitongoji ambavyo walivibaini kuwa ni Lulago, Kata ya Lwande na kingine cha Madina, Kijiji cha Kimambo, Kata ya Negero, ambako wamekamata bunduki nne aina ya magobore, bastola mbili zilizotongenezwa kienyeji, mapanga 18, shoka mbili , visu 10, madaftari yaliyokuwa yakitumika kufundishia madrasa na vitabu vya dini ya Kiislamu.

Gallawa alisema baadhi yao wakiwamo wanawake na watoto, wamechukuliwa ili kuhifadhiwa hadi hasira za wanavijiji itakapopungua kwa kuwa wamekataliwa kupokewa na ndugu zao kutokana na kile kilichoelezwa kuwa, walikuwa wakiendesha dini kwa siasa na kusababisha mateso kwa wanavijiji wasio wafuasi wa itikadi hiyo.

“Ifahamike hawa tunaowashikilia hakuna atakayeonewa wala kubambikwa makosa, ila kinachofanyika ni kuwachuja wahusikana,” alisema.

No comments:

Post a Comment

PLEASE LEAVE YOUR COMMENTS HERE. HELP BLOG DEVELOPMENT

Print It: