Digital clock

Wednesday, July 29, 2015

HOTUBA YA LOWASSA AKIJIUNGA UKAWA KUPITIA CHADEMA

Baada ya yaliyotokea Dodoma wakati wa mchakato wa kuteua mgombea Urais wa CCM, nimechukua muda kutafakari kwa kina, mustakabali wangu ndani ya Chama na Taifa kiujumla.
Watu wengi wananiounga mkono wamekuwa wakisubiri nifanye maamuzi magumu, na baada ya mashauriano marefu nimeamua kuondoka CCM kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA, kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Nimejaribu kueleza kwa kifupi sababu za kufikia maamuzi hayo, nazo ni kuwa mchakato wa kuteua mgombea wa Urais wa CCM Dodoma ulikumbwa na mizengwe na zaidi ulifanywa kwa upendeleo na chuki iliokithiri dhidi yangu.
Nimesema tena kuwa CCM niliyoiona Dodoma, sio CCM iliyonilea na kunikuza ambayo ilijengwa kwa misingi ya haki, usawa na uadilifu, na nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kudanganya nafsi yangu na watanzania kuwa nina imani na CCM kuwa chama kitakachowaletea ukombozi wa kiuchumi na kisiasa.
Wakati ninazunguka kuomba udhamini, nilieleza nia yangu kuwa ni kushirikiana na watanzania katika mchakamchaka wa maendeleo.
Bado dhamira na nia yangu ya kushirikiana nanyi ninayo, na naamini watanzania walio na imani na mimi pamoja na viongozi wenzangu wa UKAWA wataungana nasi kupambana na umaskini wa nchi hii.
Napenda kuwashukuru viongozi wa UKAWA, Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa NLD, Dr Emanuel Makaidi na Mwenyekiti wa CUF, Professa Ibrahim Lipumba kwa busara zao na kunipokea ndani ya umoja wao huu.
Pia nimetoa shukrani za dhati kwa familia yangu, viongozi na wanachama wa CCM, viongozi wa dini, makundi mbalimbali ya vijana na marafiki pamoja na watanzania wenzangu kiujumla kwa kuendelea kuniunga mkono katika kipindi chote.
Wito wangu kwa watanzania ni kuwa, tuungane kwa pamoja kuleta maendeleo kwa taifa hili, na tukumbuke wosia wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuwa watanzania wasipoyapata mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.
Mwisho, naiomba NEC iongeze muda wa kuandikisha ili ihakikishe kila mwananchi aliyeko Dar es Salaam anatimiza haki ya kujiandikisha.
Kwa machache haya naomba niwajulishe wananchi kuwa SAFARI YA MATUMAINI inaendelea rasmi ndani ya UKAWA na ninaomba mtuunge mkono.

No comments:

Post a Comment

PLEASE LEAVE YOUR COMMENTS HERE. HELP BLOG DEVELOPMENT

Print It: